Monday, 7 March 2016

Daesh: Tutaishambulia Russia kwa kulipiza kisasi


Na Renalda Mwarabu
 
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limetishia kupitia mkanda wa video kuwa, litafanya shambulio la kigaidi nchini Russia kama ulipizaji kisasi.

Katika mkanda huo uliorushwa jana katika mitandao ya kijamii, kundi hilo la kigaidi limetishia kushambulia kila mahala palipo na maslahi ya Russia kwa kile kundi hilo limesema, ni kulipiza kisasi kutokana na kuuawa wanachama wake wengi katika mashambulizi ya anga ya Russia nchini Syria.

 Mwanzoni mwa mkanda huo, Daesh sanjari na kutangaza kuhusika na mripuko ulioua polisi wawili nchini Dagestan, imeonyesha gari ililotumia kutekeleza shambulio hilo na ambalo lilikuwa limesheheni mada za miripuko. 

Aidha kundi hilo ambalo limepata hasara kubwa kufuatia mashambulizi ya ndege za Russia nchini Syria, limeonyesha likimuua mtu mmoja ambaye kwa mujibu wa Daesh, ni afisa wa upelelezi wa nchi hiyo aliyekamatwa na wanachama wa genge hilo ingawa haijabainika ukweli wake.

 Hadi sasa bado serikali ya Moscow haijatoa maelezo yoyote kuhusiana na mkanda huo wa vitisho wa kundi hilo la kigaidi.

Kwa kipindi cha miezi mitano sasa Russia, imekuwa ikiendesha mashambulizi makali dhidi ya wanachama wa kundi la Daesh na Jab'hatu Nusra nchini Syria, mashambulizi yanayotajwa kuwa na mafanikio makubwa. Chanzo Radio Terhan

No comments:

Post a Comment