Thursday, 17 March 2016

Jeshi la Cameroon laangamiza B/Haram 20 nchini Nigeria

Na Renalda Mwarabu
  
Jeshi la  Cameroon limetangaza kuwa limefanikiwa kuangamiza wanachama 20 wa kundi la kigaidi  la Boko Haram katika operesheni iliyofanyika huko kaskazini mwa Nigeria.

Kanali Jacob Kodji, kamanda mwandamizi wa jeshi la Cameroon amesema kuwa, operesheni hiyo ya jana Jumatano ya kuwaangamiza wanamgambo wa Boko Haram ilifanyika katika mji wa Djibrila, yapata kilomita 10 kutoka mpaka wa Cameroon.

 Naye Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Cameroon, Kanali Didier Badjeck amesema mateka 12 wameokolewa kutoka mikononi mwa magaidi hao sambamba na kupata silaha na magari ya kijeshi yaliyokuwa yameibiwa na matakfiri wa Boko Haram.

 Operesheni ya Jumatano dhidi ya Boko Haram imefanyika siku moja baada ya wanachama wa kundi hilo la kigaidi kuua watu 22 waliokuwa wakisali katika msikiti wa jimbo la Maiduguri, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

 Hii ni katika hali ambayo, serikali ya Benin imesema kuwa, mwezi ujao nchi hiyo itatuma kikosi cha askari 150 watakaojiunga na kile kinachoundwa na nchi kadhaa ambacho kimekuwa kikikabiliana na wanamgambo wa Boko Haram ambao wamehatarisha usalama katika nchi ya Nigeria na katika mipaka ya nchi nyengine ikiwemo Cameroon.

 Inadaiwa kuwa kuna wanamgambo 8700 wa Boko Haram kwenye eneo hilo. 

Watu zaidi ya 20,000 wameuawa na wengine zaidi ya milioni 2.5 wakilazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi tangu kundi la Boko Haram lianzishe hujuma zake nchini Nigeria mwaka 2009

No comments:

Post a Comment